WANAFUNZI WA VYUO VIKUU WASHAURIWA KUACHA BIASHARA HARAMU YA NG0N0
WANAFUNZI
wa vyuo vikuu nchini wameshauriwa kuacha kujihusisha katika biashara
zisizofaa za kuuza miili yao kwa kisingizio cha ugumu wa maisha.
Rai hiyo ilitolewa hivi karibuni na Mwenyekiti wa Shirika lisilo la kiserikali linalojihusisha
na vijana lijulikanalo kama Restless Development, Joseph Bukula,
alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika uzinduzi wa upimaji
afya kwa hiari uliofanyika katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
Bukula
alisema vijana wanachotakiwa kufanya kwa wakati huu ni kuhakikisha kuwa
wanajitambua kwa kufanya kile kilicho wapeleka chuoni na si kujiingiza
katika biashara zisizofaa na zinazoshusha maadili yao.
Alibainisha kuwa vijana wengi hasa waliopo katika vyuo mbalimbali
wamekuwa wakiingia katika mitego inayowapelekea kujikuta wakipata
maambukizi ya virusi vya Ukimwi kutokana na wao kushindwa kujitambua.
"Kijana kama atajitambua anaweza kufanya mambo yake bila hofu yoyote pia
haitakuwa rahisi kwa yeye kudanganyika kwani kujitambua kwake
kutamjengea kujiamini," alisema Bukula.
Aidha alisema bado kuna changamoto kubwa ya elimu kwa vijana juu ya
masuala ya upimaji Ukimwi kwa hiari kutokana na kutokwepo kwa idadi
kubwa ya watu wanaojitokeza.
Alisema lengo la kuendesha zoezi hilo la upimaji katika chuo hicho ni
kuwasaidia vijana kutambua afya zao pia kupata elimu ya maambukizi hayo
na kuweza kujikinga.
"Restless inatoa elimu kwa vijana juu ya ugonjwa wa Ukimwi kwa vijana wa
chuo hiki lakini ambapo pia tumezindua bango chuoni hapa lenye ujumbe
kwa jamii linalosema eneza elimu na si virusi," alisema Bukula.
Naye Mratibu wa miradi wa shirika hilo Selestine Ngowi, alisema kuwa
mradi huo wa kutoa elimu kwa vijana utakuwa endelevu ili kuweza
kuwasaidia vijana walioko chuoni na mitaani kuweza kujikinga na virusi
vya Ukimwi.
Ngowi alisema kuwa pia wamekuwa wakitumia njia mbalimbali ikiwemo redio
kuwafikishia vijana elimu inayohusu masuala ya virusi vya Ukimwi na
Ukimwi ili kuweza kupunguza maambukizi mapya kwa vijana.
-Habari leo
0 comments: