HASHIM LUNDENGA, NINGENG’ATUKA MISS TANZANIA


Mkurugenzi wa Lino Agency ambao ni waandaaji wa Miss Tanzania, Hashimu Lundenga. akifafanua 
Kwako, Hashim Lundenga.
Ni matumaini yangu kwamba hunifahamu licha ya kwamba majina yetu yanashabihiana. Najua jinsi jasho linavyoendelea kukutoka kutokana na changamoto kubwa unazokutana nazo, tangu ulipomtangaza Sitti Mtemvu kuwa Miss wa Tanzania 2014.
Mimi si Mkurugenzi wa Lino International Agency, kampuni inayoendesha mashindano ya Miss Tanzania kwa mwaka wa 18 sasa mfululizo. Mimi sijawahi kwenda Wizara ya Elimu na Utamaduni (kipindi hicho) kuomba kibali cha kuyaanzisha tena mashindano ya Miss Tanzania baada ya kuwa yamepigwa marufuku kwa zaidi ya miaka 24 (yalipigwa marufuku mwaka 1968 kutokana na sababu za kimaadili).
Sikushirikiana na Prashant Patel kumtafuta mkurugenzi wa utamaduni kipindi hicho, Baya Senkemwa na kumuomba ‘chondechonde’, aangalie kama kuna namna tunayoweza kuruhusiwa kuirudisha Miss Tanzania.
Mimi ni mlalahoi tu ambaye sina ubavu wa kufanya kama wewe uliyoyafanya. Nakuhakikishia, tangu kipindi hicho, mimi nisingekuwa na ubavu wa kuendelea kusimamia mashindano hayo na kutoa warembo kedekede kwa zaidi ya miaka 18 kama wewe, ningeanzia wapi?
Hata hivyo, hayo yote hayanizuii kukufikishia ujumbe wangu kwako, anko wahenga wanasema, nguo ikimvuka muungwana huchutama. Jahazi la Miss Tanzania linazama anko, ng’atuka ili uendelee kutunza heshima yako.
Kwa uzoefu na uelewa wako, najua unajua fika kwamba mwaka huu ‘umebugi’ kumtangaza Sitti Mtemvu kuwa Miss Tanzania. Sijui kama ni urafiki wa kawaida kati yako na baba yake, mheshimiwa Abbas Mtemvu uliokusukuma kumpa ushindi au ni vigezo alivyokuwa navyo msichana huyo, sitaki kuzungumzia huko, ishu kubwa hapa ni suala la umri.
Yawezekana awali hukujua kama umeingizwa chaka na Sitti kwa kukuletea cheti chenye utata kuhusu umri wake halisi. Huenda wewe na kamati yako mlijiridhisha kwamba kweli Sitti alizaliwa mwaka 1991. Katika hili mnaweza kusamehewa kwamba ‘huenda’ hamkuujua ukweli mapema.
Hata hivyo, kama kweli mliingizwa chaka, iweje hata uthibitisho mwingine ulipopatikana wa hati ya kusafiria ya Sitti yenye namba AB201696 kuonesha kwamba mrembo huyo alizaliwa Mei 31, 1989 na siyo 1991 kama alivyowaaminisha, kwa nini mnaendelea kuwa wagumu na kushikilia msimamo wa awali?
Hapa naanza kupata shaka Lundenga, nilitegemea kwamba kwa sababu umepata uzoefu wa kutosha wa kuongoza Miss Tanzania kwa miaka 18, ungeweza kung’amua haraka kwamba kelele anazopigiwa Sitti kuhusu kudanganya umri zina hoja ndani yake.
Badala ya kuendelea kutetea ubatili wa Sitti, ungesimamia kwenye ukweli na kuwaeleza Watanzania kwamba mlighafirika na kumpa ushindi mtu asiyefaa kwa sababu aliwadanganya.
Badala yake, umeendelea kumtetea huku ukishindwa hata kugundua kwamba kujikanyaga kwa mrembo huyo wakati akihojiwa na waandishi wa habari, ilikuwa ni kwa sababu kuna jambo analificha.
Hapana Lundenga, hapa umechemka na kwa kuwa unaendelea kutetea uovu, unazidi kutupa shaka zaidi. Nikwambie tu, inaonekana unafahamu kila kitu kuhusu mchezo unaoendelea na hiyo pekee inatosha kukuondolea sifa za kuwa hapo ulipo.
Kwa bahati mbaya mimi nitabaki kuwa mimi na sitaweza kuwa wewe lakini kama ningekuwa mimi kwenye nafasi yako, kwa hili la Miss Tanzania 2014, narudia tena kusema bila kumung’unya maneno kwamba ningeng’atuka na kuwaachia wengine wenye uwezo zaidi yangu waongoze Miss Tanzania.

0 comments: