Maiti yakaa mochwari siku 34, kisa mgogoro wa wazazi



Moshi. Mgogoro mwingine mkubwa wa kifamilia wa kugombea maiti, umeibuka mjini Moshi na kusababisha mwili wa Rosemary Marandu (38), kuhifadhiwa mochwari kwa siku 34.
Mwili wa marehemu huyo aliyefariki dunia Septemba 4, mwaka huu umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC na umekuwa ukilipiwa Sh9,000 kwa siku, hivyo siku 34 gharama yake imefikia Sh306,000.
Tukio hilo limekuwa gumzo mjini Moshi hasa baada ya kutokea siku chache baada ya maiti nyingine ya Steven Assey kufukuliwa kwa amri ya Mahakama na hadi leo ni siku ya 29 bado haijazikwa licha ya mke mdogo wa marehemu, Fortunata Lyimo kupewa haki ya kuzika lakini amekataa akisema ni kinyume cha mila na utamaduni wao kwa mtu kuzikwa mara mbili. Akizungumza jana, mama mzazi wa Rosemary Marandu, Felicia Nkya, alidai kuwa mumewe aitwaye Flavian Marandu ndiye anayeshikilia mwili huo hadi leo.
Marandu ni Diwani wa Kata ya Mrao Keryo kwa tiketi ya CCM na anamiliki vitega uchumi kadhaa vikiwamo viwanda vya kupasua mbao na nyumba za kulala wageni.
“Ukweli ni kwamba tangu amekufa (Marandu) hajatupa taarifa yoyote zaidi ya kunitumia meseji ya simu akiniuliza kama mume wa Rosemary ameniambia kama Rosemary amekufa. Kwa mila na utamaduni wetu, mtu akifa tunakaa pamoja na kupanga mazishi lakini hadi leo hajatuma mtu yeyote kuzungumza na sisi juu ya msiba.”
Felicia alisema walitengana na mumewe huyo mwaka 1982 na mtoto wao huyo amezaa watoto wanane na wanaume tofautitofauti na mumewe aliyemfia, Sigfrid Mlingi naye amezuiwa kumzika.
“Naumia sana napata mateso makubwa ya kiakili na kisaikolojia. Mwezi mzima sasa sijui hatima ya mazishi ya mtoto wangu. Hakuna chakula kinachopita naomba mnisaidie jamani,” alilalamika.
Mama huyo alidai kuwa awali walikwenda kulalamika polisi ambako walishauriwa kufungua shauri mahakamani lakini akadai kwamba hawana nguvu ya kushindana na Marandu.
“Tumeamua kumkabidhi Mungu kwa sababu hatuwezi kushindana naye (Marandu) tukamshinda. Hata kule KCMC anadai kuna kesi mahakamani lakini sisi hatujafungua kesi,” alidai.
Mumewe azungumza
Mlingi alisema ameamua kujiweka kando kushughulikia mazishi ya mkewe baada ya baba mkwe kumtolea lugha isiyofaa.

“Mimi ndiye nilimuuguza hapo Mawenzi mpaka akanifia mikononi mwangu na baada ya kufa nilikwenda Keryo na kuonana na baba yake lakini akanifukuza,” alidai Mlingi.

0 comments: