LIPUMBA: KWANZA CCM ING’OKE, RUZUKU BAADAYE
Wakati Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi akisema suala la ruzuku na viti maalumu ni changamoto kwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba amesema hicho si kipaumbele.
“Tunachokitaka
ni kuunganisha nguvu zetu ili kuhakikisha tunaing’oa CCM madarakani
kwanza, masuala mengine kuhusu ruzuku tutaweka utaratibu maalumu
baadaye,” alisema.
Profesa
Lipumba ambaye pia ni mwenyekiti mwenza wa Ukawa, alisema hayo Dar es
Salaam jana alipokuwa akiwaeleza waandishi wa habari maazimio ya Baraza
Kuu la Uongozi la Taifa la CUF lililokutana Jumatatu na Jumanne
iliyopita.
“Wenzetu
Kenya waliweza kuungana na kuhakikisha wanaking’oa chama tawala
madarakani, lakini sasa kwa hapa mkiungana na kuwa chama kimoja ni
lazima msajili chama chenu, sasa tunachokitaka ni kushirikiana tu
kwanza,’’ alisema.
Alisema
suala la ruzuku na uteuzi wa viti maalumu siyo lengo kuu la Ukawa
inayoundwa na vyama vinne; CUF, Chadema, NCCR-Mageuzi na NLD kwa kuwa
linajadilika. Alisema jambo la msingi hivi sasa ni ushirikiano wa amani.
Alisema
kinachotakiwa kwa viongozi wa Ukawa ni kuaminiana kwanza ili kulinda
muungano huo ambao alisema umeshaanza kukitikisa chama tawala, CCM.
Maazimio ya Baraza Kuu
Alisema
Baraza hilo lilisisitiza umuhimu wa kuaminiana miongoni mwa vyama
washirika katika ngazi zote ili kudumisha umoja huo na kufikia lengo la
kuitoa CCM madarakani.
“Baraza
limetaka uwepo utaratibu mzuri na wa wazi utakaoonyesha mambo ya msingi
ambayo vyama vinavyounda Ukawa vimekubaliana. Utaratibu huu uwafikie
viongozi wa ngazi zote za chama ili kuhakikisha jukwaa la Ukawa
linatumika kwa lengo na dhamira iliyopo ndani ya hati ya makubaliano
ambayo ni kuing’oa CCM madarakani,” alisema.
Kuhusu
uchaguzi wa Serikali za Mitaa Profesa Lipumba alisema Baraza limetaka
sheria irekebishwe ili uchaguzi wa diwani ufanyike pamoja na wa viongozi
wa mitaa, vijiji na vitongoji kwa wakati mmoja, kwa vile diwani ndiye
kiongozi mkuu wa kuchaguliwa wa kata.
Baraza
hilo pia limetaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), iratibu na kusimamia
uchaguzi wa Serikali za Mitaa na utengenezwe utaratibu ambao utaifanya
Tume hiyo kuwa huru kuwezesha chaguzi zote zijazo kufanyika kwa uhuru na
haki.
“Taarifa
za Tume zilieleza kuwa itaandikisha wapigakura mpaka kwenye ngazi ya
vijiji na vitongoji, kwa hiyo uchaguzi wa Serikali za Mitaa usubiri
mpaka daftari la kudumu la wapigakura likamilike na ndilo litumiwe
kwenye uchaguzi huo,” alisema.
Akizungumzia
Katiba Inayopendekezwa, Profesa Lipumba alisema Baraza Kuu la CUF,
limesikitishwa kwa kiasi kikubwa na kitendo cha kupitishwa na kutangazwa
kwa katiba hiyo na Bunge la Katiba lililoongozwa na Samuel Sitta
akisema halikuzingatia sheria na taratibu za mabunge ya Jumuiya ya
Madola.
“Ni
ukweli usiofichika kwamba mchakato mzima wa kupitisha katiba haukuwa na
mwafaka wa kisiasa, kanuni za uendeshaji wa bunge hilo zilikiukwa na
Katiba yote inayopendekezwa haikupigiwa kura ya mwisho,” alisema
Profesa
Lipumba alisema, katika vikao vya ushauriano na viongozi wa vyama vya
siasa vinavyounda Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), Rais Jakaya
Kikwete alikubaliana na viongozi hao kuwa mchakato wa kupata Katiba
Mpya, hususan kura ya maoni uahirishwe mpaka baada ya Uchaguzi Mkuu
2015.
“Mwanasheria
wa Serikali alitangaza kura ya maoni Machi 30, Rais akiwa China alisema
Aprili, yaani tayari tarehe imeshatangazwa kabla hata ya daftari la
wapigakura kukamilishwa,” alisema.
Alisema
baraza hilo pia limesikitishwa na utaratibu unaofanywa na NEC juu ya
uboreshaji wa Daftari la kudumu la Wapigakura akisema hadi sasa hatua za
uandikishaji hazipo wazi na wadau wengi hawana taarifa za kutosha juu
ya nini kinaendelea.
Alisema
takwimu za Sensa ya Watu na Makazi 2012, zinaonyesha kuwa kuna vijana
zaidi ya milioni 4.6 ambao watafikisha umri wa kuwa wapigakura kabla ya
Uchaguzi Mkuu wa 2015 lakini bado hawajapewa fursa ya kuandikishwa huku
wananchi wengi wakiwa wameshapoteza vitambulisho vya kupigia kura.
Alisema
Juni, 19 mwaka huu, Nec, ilitangaza kufuta matumizi ya vitambulisho vya
kupigia kura vya sasa na badala yake itatumia teknolojia mpya ya
Biometric Voter Registration (BVR), ikiwa ni maboresho ya daftari la
kudumu la wapiga kura na kwamba Mwenyekiti wa Nec, Jaji Damian Lubuva
alinukuliwa akisema katika Kura ya Maoni ya Katiba na Uchaguzi Mkuu,
mpigakura atatumia kitambulisho kipya baada ya kuandikishwa upya katika
mfumo huo na si vinginevyo.
Pia
alisema Baraza Kuu linalaani vitendo vya uvunjifu wa haki za binadamu
na sheria vinavyoendelea kufanywa na Serikali kwa kulitumia Jeshi la
Polisi.
Alitoa
mfano wa masheikh waliokamatwa Zanzibar na kuhamishiwa Dar es Salaam na
kufunguliwa kesi akisema walijitokeza mbele ya Mahakama na kusema
waziwazi kwamba wamefanyiwa mateso na vitendo vya kinyama lakini hakuna
hatua zilizochukuliwa ikiwamo kupelekwa hospitali.
Kadhalika,
alisema baraza hilo limepokea kwa mshangao taarifa za utoaji wa uraia
unaofanywa na Serikali kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi.
Alisema uamuzi wa kuwapa uraia wakimbizi katika majimbo yanayoongozwa na
wabunge wa vyama vya upinzani ni mbinu ya kudhoofisha upinzani kwa kuwa
wakimbizi wanaopewa uraia wanahamasishwa kuwa wachague chama tawala.
Kuhusu
ardhi alisema: “Pamoja na Tanzania kuwa na ardhi ya kutosha kwa raia
wake, ugawaji wa mapande makubwa ya ardhi kwa wawekezaji yataleta
mtafaruku wa uvunjifu wa amani na kuwafanya raia wazawa kuwa maskini wa
kudumu,’’ alisema Profesa Lipumba.
Kuhusu
maradhi hatari ya ebola, Profesa Lipumba alisema Baraza Kuu limeitaka
Serikali kuwa makini ili usiingie nchini akisema limesikitishwa na
taarifa ya kwamba mpaka sasa nchi haina vifaa vya kuthibitisha kuwapo
kwa vimelea vya ebola.
Chanzo: Gazeti la Mwananchi
Chanzo: Gazeti la Mwananchi
0 comments: