UNAJUA WANAUME WANAPENDA KUOA WANAWAKE WA AINA GANI??
Habari za wiki hii mpenzi msomaji. Mimi
namshukuru Mungu kwa kuweza kunikutanisha na nyinyi kupitia safu hii
ambayo pamoja na mambo mengine nazungumzia juu ya mada mbalimbali ambazo
zinagusa maisha yetu ya kila siku.
Wanaume wengi wanapofikia hatua ya kuoa
si kwamba wanakurupuka tu na kuoa mwanamke yeyote mwenye sura nzuri,
bali huchukua muda wao mwingi kuchunguza mambo mengi juu ya wake ambao
wanadhani kwamba wanaweza kuwa pamoja kwa kipindi chote cha maisha.
Wanawake wengi wanajisahau na kudhani
kwamba kitu kinachoweza kuwafanya wakapata wachumba ni uzuri hivyo
kupoteza muda wao kujichubua na kujiremba ili wawavutie wanaume bila
kujua kwamba kuolewa ni zaidi ya uzuri.
Hali sasa hivi imebadilika ni tofauti
na kipindi cha nyuma ambapo ukiwa na sura nzuri na umbo la kuvutia basi
una asilimia 100 za kuolewa.
Utafiti ambao nimeufanya unaonesha
kwamba zaidi ya uzuri wa tabia na umbo, kuna kuna sifa nyingine za
msingi ambazo mwanamke anatakiwa kuwa nazo ili aweze kuwa katika
mazingira mazuri ya kupata mchumba wa kumuoa kiasi kwamba asipokuwa nazo
ataishia kuchezewa tu lakini haitatokea mtu kumtakiwa kwamba anataka
kumuoa.
MWEYE MAPENZI YA KWELI
Lengo kubwa la mwanaume kuoa ni kutaka
kupata mapenzi ya kweli kutoka kwa mwanamke na ikiwezekana waweze kupata
watotoa ambapo watoto mara ndio wamekuwa furaha ya ndoa. Wapo wanawake
wengine ambao wanonesha wazi kutokuwa na mapenzi ya kweli bali wanakuwa
na mapenzi ya kuzuga. Wanachotaka wao aidha kupata umaarufu tu kwamba
yuko na mtu fulani ama kuweza kupata pesa alizonazo mwanaume lakini sio
kwamba ana mapenzi ya dhati kutoka moyoni mwake.
Mwanamke asiye na mapenzi ya dhati
utamgundua tu, muda mwingi utamuona macho yake yako kwenye mfuko wa
mwanaume. Akiona kwamba mfuko umetuna utaona anaonesha mapenzi ya hali
ya juu lakini pindi hali inapokuwa kubwa mbaya kifedha mapenzi yanaanza
kufifia.
Kwanini wanaume wanapenda wana wake
wenye mapenzi ya dhati kutoka mioyoni mwao na si kutokana na fedha
walizonazo? Hii inatokana na ukweli kwamba maisha siku zote
yanabadilika, kama waswahili wanavyosema, kuna kupanda na kushuka.
Sio kwamba kila siku utakuwa na maisha
mazuri na kama itatokea hivyo basi ushukuru mungu.Hivyo basi mwanamke wa
kuoa lazima afahamu hivyo na awe tayari kuonesha mapenzi yake ya dhati
wakati wote wa maisha yao na si kwa kipindi fulani tu cha neema.
Si hivyo tu pia asilimia kubwa ya
maisha ya ndoa yanatawaliwa na mapenzi, kwa hiyo nyanja hiyo inakuwa ya
msingi sana kwa wanaume wengi kuiangalia ili wasije wakajikuta wanaoa
mwanamke ambaye baada ya muda mapenzi yanakwenda likizo hali ambayo
inaweza kuwafanya wasiishi maisha ya raha mustarehe.
WENYE TABIA NZURI
Tabia njema ndio silaha ya maisha,
ukiwa na tabia nzuri kila mtu atakupenda, hiyo ni katika maisha ya
kawaida. Lakini linapokuja suala na kuoa tabia inakuwa kitu cha awali
sana kungaliwa na hiyo inaweza kuwa na ukweli kwa sababu wapo wasichana
wazuri wenye mvuto wa aina yake na maumbile mazuri, lakini wanakosa
wanaume wa kuwaoa, ukiuliza kwani utaambiwa anatabia mbaya.
Naweza kusema hilo ndilo limekuwa
tatizo kubwa kwa baadhi ya wanawake kukosa wanaume wa kuwaona. Hakuna
mwanaume hata mmoja kati ya wale ambao nimejaribu kuongea naye ambaye
ameonesha kulidharau suala hilo la tabia.
Si hivyo tu wapo wanaume ambao
wameingia kichwa kichwa na kuoa kwa kuangalia sura tu bila kujali tabia,
matokeo yake baada ya siku chache yanatokea machafuko ya aina yake hali
ambayo imepelekea kuvunjika kwa ndoa kutokana na tabia mbaya alizonazo
mwanamke.
WENYE UCHU NA MAENDELEO
Hivi karibuni kumekuwepo na mabadiliko
ya aina yake kwa wanaume, wengi sasa hivi hawapendi kabisa kuoa mwanamke
ambaye hana kazi yaani 'golikipa'. Kama atakuwa hana kazi basi awe na
uchu wa maendeleo kwa kujituma kufanya kazi mbalimbali za kimaendeleo
kama vile kilimo kwa wale walio vijijini na biashara ndogondogo kwa wale
ambao wako mijijini na hata vijijini.
Ile dhana ya kusema mwanamke ni mama wa
nyumbani wa kukaa na kujipodoa akimsubiria mwnaume arudi amstarehesha,
sasa hivi imepitwa na wakati. Wanaume wengi wanapenda wanawake ambao ni
wahangaikaji, wenye ndoto za maendeleo katika maisha yao. Hata kama
watakuwa si wafanyakazi lakini wawe wenye kutoa ushauri kwa waume zao
juu ya jinsi gani wafanye ili wafanikiwe.
WASIOPENDA MAKUU
Kuna wanawake wengine wanakuwa na
tabia za ajabu sana kiasi kwamba yaweza kuwa kero kwa wanaume. Wapo
wanawake ambao wanapenda makuu bila kujali hali halisi ilivyo. Kuna
wanawake naweza kusema wana tamaa, kila wikiendi utamsikia "leo
tunakwenda wapi dear?"
Akimuona rafiki yake kanunua simu ya
laki tatu na yeye utamsikia akisema, ‘na mimi naomba uninunulie simu
kama ya Grace’. Ukienda naye Pub anakuambia, "mimi sinywi pombe za
chupa natumia za kopo tena Heineken’. Yeye hajali kiasi cha pesa
mwanaume alicho nacho na usipotekelezea anachukia na anaweza hata
kupunguza mapenzi.
Wanawake kama hawa wako katika
mazingira magumu sana ya kuweza kupata wanaume wa kuwaoa. Mara nyingi
katika maisha fedha huzungumza, kama mwanaume atakuwa na pesa ya kutosha
itakuwa rahisi sana kwa mwanamke kupata kila atakachopenda lakini si
kwa kumwambia mimi nataka kitu fulani.Mwanaune mwenyewe utamsikia
akisema, ‘unataka nikununulie simu ya aina gani, au leo unataka twende
wapi?’ hapo ndipo utakuwa na nafasi ya kusema, ‘mimi nataka uninunulie
simu kama ya fulani ama leo nataka twende sehemu fulani.’
Wanaume ni warahisi sana wa kuwapatia
wale ambao wanatarajia kuwaoa chochote ambacho watahitaji kama tu pesa
haitakuwa tatizo. Kitu ambacho kinawaudhi wanaume wengi ni ile tabia
ya mwanamke kupenda mambo makubwa bila kuangalia uwezo uliopo kwa
mwanume.
Kuna wanawake wengine wao si wasemaji
kabisa, yeye anasubiri leo amemletea hiki, anapokea na kushukuru, kesho
akiambiwa twende beach anakubali. Au wengine wanasubiri mpaka waulizwe
wanataka nini, ndio wanasema.
Sisemi kwamba uwe mkimya tu hata kama
una shida ya kitu fulani na unafahamu kwamba ukimweleza mwenza wako
anaweza kukusaidia, hapana! kama unaona kwamba uwezekano wa kupata kile
ambacho unakihitaji upo mweleze kwa utaratibu naamini atakuelewa na
kukutimizia.Tabia ambayo hawaipendi wanaume wengi ni ile ya kulazimisha
ufanyiwe kitu fulani wakati inawezekana uwezekano haupo.
WAVUMILIVU
Wapo wanawake ambao sio wavumilivu
kabisa katika maisha.Tunajua kwamba maisha siku zote hayatabiriki,
yanaweza kutokea matatizo ya kiafya ama kifedha.Huu ndio wakati wa kuona
uvumilivu wa mtu.Kama mwanamke anatarajia kwamba siku zote ni za raha
tu na pindi matatizo yanapotokea anachukua uamuzi wa kumtoroka mwanume,
huyo siyo mwanamke wa kuoa.
Wangapi leo hii huwatoroka waume zao
pindi inapotea kuumwa, kufilisika ama kupatwa na tatizo lolote ambalo
kwa namna moja ama nyingine yanaweza kuwafanya maisha yao kutingishika?
Uvumilivu kwa mwanamke utakuwepo kama
tu atakuwa na mapenzi ya dhati kama nilivyozungumza hapo awali. Mwanamke
mweye mapenzi ya dhati ni lazima atakuwa mvumilivu na atakuwa tayari
kuishi katika maisha ya aina yoyote, yawe ya raha ama ya starehe.Hawa
ndio wale ambao wanaume wengi wengependa kuwa nao maishani mwao.
Licha ya kupenda kuoa wanawake amabo
wana tabia hizo nilizozitaja hapo juu, wanachukizwa sana na wanawake
ambao wanavijitabia vidogo vidogo ambavyo kimsingi havikubaliki katka
jamii.
Tabia hizo ni kama wambea, wasio
wakweli na wawazi, wasioridhika, wagumu kusamehe na wapesi wa kuchukia,
wagomvi na wenye roho ya kwanini.
Utafiti huu umefanyikwa kwa baadhi ya
wanaume ambao wanatarajia kuoa wanawake ambao wanaoishi katika maeneo
mbalimbali jijini Dar-es-Salaam.
Kwa maana hiyo basi hiyo iwe changamoto kwa wanawake. Wajue kwamba wanaume wanafurahi kuwa na wanawake wa aina gani. Hata kama utakuwa umeshaolewa, kama kuna wakati kunakuwa na kutokuelewana baina yenu, chunguza yawezekana kwamba unakosa mojawapo ya tabia ambazo nimezitaja hapo juu. Waweza kubadilika kwani inawezekana.
Kwa maana hiyo basi hiyo iwe changamoto kwa wanawake. Wajue kwamba wanaume wanafurahi kuwa na wanawake wa aina gani. Hata kama utakuwa umeshaolewa, kama kuna wakati kunakuwa na kutokuelewana baina yenu, chunguza yawezekana kwamba unakosa mojawapo ya tabia ambazo nimezitaja hapo juu. Waweza kubadilika kwani inawezekana.
0 comments: