Waziri Nyalandu: Nitachukua Uamuzi Mgumu Muda Ukifika


Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu amesema anaamini kuwa rais ajaye wa Tanzania, atakuwa ni kijana na kusema kwamba kila zama zina kitabu chake.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili hivi karibuni, waziri huyo alisema kuwa itakuwa ni kosa iwapo Rais Jakaya Kikwete atakabidhi kijiti kwa mtu mwenye umri unaofanana naye.

Nyalandu alibainisha kwamba wakati ukifika, atatangaza iwapo atagombea urais au kuendelea kugombea ubunge katika jimbo lake la Singida Kaskazini.

“Ukifika wakati ni lazima kubadilishana vijiti. Ni lazima kizazi kinachomaliza muda wake, kikabidhi kijiti kwa kizazi kinachofuata. Ni wazi mtu mwenye umri unaofanana na kiongozi anayeondoka madarakani hana nafasi,” alisema Nyalandu akiongeza:

“Kijiti hiki anachokiacha Jakaya Kikwete, aliachiwa na kaka yake Rais Benjamin Mkapa na Mkapa naye aliachiwa kijiti na kaka yake Mzee Ali Hassan Mwinyi ambaye ndiye alisema kila zama na kitabu chake.”

Alieleza kuwa huo ni uhalisia wa maisha na kwamba ni lazima kila mtu kukubali hivyo.

“Sasa tunahangaika kuandika hitimisho la zama za Rais Kikwete, ndiyo sisi tunapambana kuhakikisha tunakomesha ujangili na wengine wanafanya kazi nyingine. Haya yakikamilika ni zama zake (Rais Kikwete), zimekamilika,” alisema Nyalandu.

Alifafanua: “Rais Kikwete atakabidhi kitabu kwa zama nyingine na sharti akabidhi kijiti kwa kizazi kinachofuata. Haitawezekana ikiwa atakabidhi kijiti kwa kizazi chake hichohicho. Ni kosa kurudia zama zilizopita.”

Nyalandu alisema kuwa ni vyema mtu yeyote mwenye umri unaofanana na kiongozi anayeondoka madarakani akasahau kupewa kijiti kwani historia na hata maandiko ya Mungu vipo tofauti.

0 comments: