MAJAMBAZI YAPORA SH1 BIL STANBIC
Makao makuu ya Benki ya Stanbic yaliyopo Wilaya ya Kinondoni, barabara ya Alli Hassan Mwinyi jijini Dar es Salaam.
Watu 13 wakiwamo wafanyakazi tisa wa
Benki ya Stanbic jijini hapa wanashikiliwa na polisi baada ya majambazi
kuiba fedha zaidi ya Sh1 bilioni jana jioni.
Watu hao wanashikiliwa katika Kituo cha
Oysterbay kwa uchunguzi zaidi wa uporaji huo uliofanywa na majambazi
yenye silaha yaliyoingia katika Tawi la benki hiyo la Mayfair Plaza
lililopo Barabara ya Mwai Kibaki na kutokomea na kitita hicho.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni,
Camillius Wambura, aliliambia gazeti hili jana kuwa watu wengine wanne
wanaoshiliwa ni askari aliyekuwa lindo na wengine watatu ambao hakuwa
tayari kuwataja.
Wambura ndiye aliyeongoza kikosi cha
askari kanzu na wenye sare kufanya uchunguzi wa awali katika jengo la
benki hiyo ili kujiridhisha na kilichotokea katika tukio hilo. Alisema
kiasi kamili cha fedha zilizoibwa kitatolewa baadaye baada ya polisi
kukamilisha uchunguzi wao.
“Siwezi kusema leo moja kwa moja kiasi
kamili cha fedha zilizoibwa kwa sababu kila mmoja tuliyemhoji anatoa
kiwango tofauti,” alisema Wambura.
Hata hivyo, chanzo chetu cha habari
ambacho hakikutaka kitajwe gazetini, kilidai kuwa hadi jana alasiri,
maofisa wa benki hiyo waliokuwa wanashiriki uchunguzi, walibainisha kuwa
kiasi cha zaidi ya Sh1.0943 bilioni kilikuwa kimeibwa.
Chanzo hicho kilibainisha kuwa kiwango
hicho cha fedha kinajumuisha sarafu mbalimbali zikiwamo fedha za
Tanzania, Euro, Pauni na Dola za Marekani.
Habari zilizopatikana baadaye kutokana
katika chanzo chetu, zilidai kuwa fedha zilizoibwa ni Euro 260,000
(Sh598 million), Dola za Marekani 175,000 (Sh280milioni), Sh216 milioni
za Tanzania, na pauni 190 za Uingereza (Sh380,000).
0 comments: