RAY C:NIMEMSAMEHE CHID BENZ NA KUMFUTIA KESI
WAKATI nyota wa muziki wa Hip Hop, Rashid Makwiro ‘Chid Benz’ akikamatwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere akiwa na madawa ya kulevya akiwa njiani kuelekea Mbeya, Rehema Chalamila ‘Ray C’ aliyekuwa amemfungulia kesi ya kumpiga katika kituo cha Polisi cha Oysterbay, amefuta shauri hilo na kumsamehe.
Akipiga stori na gazeti hili, Ray C
alisema ameamua kumsamehe kwa sababu yeye ni mtu wa Mungu na anaamini
yanayomtokea ni ishara ya kumtambulisha kuwa matumizi ya dawa za kulevya
hayafai.
“Mimi ni mtu wa Mungu, nimemsamehe na
wala sitaki kesi naye, lakini kumsamehe mimi peke yangu hakusaidii,
Watanzania wote kwa pamoja tumuombee ili jambo hili limalizike na
likiisha, ninamuomba aje tushiriki pamoja katika tiba ya Methadone,”
alisema.
Ray C maarufu kama kiuno bila mfupa,
alitoa kauli hiyo muda mfupi baada ya kuandika waraka katika akaunti
yake kwenye mtandao wa Instagram, akimsihi Chid Benz kuachana na
matumizi hayo ya madawa ya kulevya.
“Pole kaka yangu Chid Benz, naumia kuona
tatizo ulilokuwa nalo bado haujalitafutia jibu, mimi ni dada yako na
tumeshafanya kazi pamoja. Tatizo ulilonalo na mimi nilishakuwa nalo na
niliweza kulitatua sababu nilijitambua na kutafuta suluhu, nimejaribu
kila njia kukushauri badala yake ukaja na rungu la kimasai na
kunitandika nalo nyumbani kwangu,” yalisomeka baadhi ya maandishi yake
mtandaoni.
Chid Benz alikamatwa akiwa na kete 14 za
madawa ya kulevya pamoja na misokoto miwili ya bangi hadi gazeti hili
linakwenda mtamboni, alikuwa bado hajafikishwa mahakamani kukabiliana na
tuhuma hizo.
0 comments: