UKATILI..!! MWANAMKE ACHINJWA NA KUNYOFOLEWA SEHEMU ZA SIRI
Watu wasiofahamika wamemuua kwa kumkata mapanga na kisha kumnyofoa sehemu zake za siri mkazi wa Kijiji cha Kanegele, wilayani Mbogwe, Mkoa wa Geita, Hollo Machibula (54).
Akizungumza
kijijini hapo juzi, Diwani wa Kata ya Bukandwe, Henry Alphonce alisema
Hollo alivamiwa na watu hao nyumbani kwake juzi saa 5:00 usiku akiwa
amelala na kuanza kumkatakata kwa mapanga.
Alphonce
alisema mwanamke huyo alikuwa akiishi na binti yake, Tatu Juma (25)
ambaye wauaji hao walimlazimisha kuingia chini ya uvungu wa kitanda
kabla ya kuanza kumshambulia mama yake.
Alisema alipata
taarifa za tukio hilo saa 6:00 usiku baada ya kupigiwa simu na viongozi
wa kitongoji waliofika eneo la tukio na kushuhudia mauaji hayo.
Mtoto
huyo alisema alishuhudia jinsi mama yake alivyokuwa akichinjwa na
kunyofolewa sehemu zake za siri walizotoweka nazo wauaji hao.
“Waliniamrisha
nilale chini nisiwaagalie usoni, walipomaliza kumchinja mama walikimbia
na mimi nikapata mwanya wa kupiga kelele kuomba msaada nikiamini kuwa
mama atakuwa kaumizwa tu hajafa,” alisema Tatu.
Baadhi
ya wakazi wa eneo hilo walidai kuwa huenda chanzo cha mauaji hayo ni
migogoro iliyokuwapo kwenye ndoa ya binti yake na mumewe.
Inadaiwa
kuwa Tatu alikorofishana na mumewe ambaye hawakumtaja jina na mume huyo
alipokuwa akienda nyumbani hapo kumtaka arudi nyumbani kwake, mama yake
alikuwa akimkataza binti huyo asirejee kwa mumewe.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Geita, Joseph Konyo alisema wanamshikilia mtu mmoja
kwa mahojiano na wanaendelea kuwasaka wale wote waliohusika na mauaji
hayo.
Alitoa wito kwa wakazi wa eneo hilo kuisaidia Polisi kuwasaka wauaji hao.
0 comments: