DARASA LA WAKUBWA..!..WANAPENDANA, WEWE UNAWAFITISHA WAACHANE ILI UPATE NINI?

Namshukuru Mungu kwa kunifanya niione wiki hii nikiwa mzima wa afya huku nikiendelea vyema na shughuli zangu za kila siku kama kawaida. Natumaini nawe hujambo na uko tayari kukisoma kile nilichokuandalia.
Hata hivyo, kabla ya kwenda kwenye mada ya leo, niwashukuru sana wasomaji wangu ambao wamekuwa wakinitumia sms na wakati mwingine kunipigia kunipongeza kwa yale ambayo nimekuwa nikiyaandika kupitia ukurasa huu.
Namshukuru sana mama Zuhura wa Kibaha ambaye kila ninapotoa mada amekuwa msitari wa mbele kunipongeza na kunikosoa pale inapobidi. Lakini huyu ndiye aliyenifanya niandike mada yenye kicha cha habari kilichopo hapo juu.
Mpenzi msomaji wangu, huko mtaani kuna watu ambao wanajua kupendana. Yaani kutokana na mapenzi ya dhati waliyonayo, wanajikuta wakiishi kwa furaha na amani huku kila mmoja akijisikia wa kipekee.
Kwa ulimwengu wa sasa ukitokea kumpenda mtu na yeye akaonekana kukupenda umshukuru sana Mungu. Hii ni kwa sababu, mapenzi ya sasa yamejaa usanii mwingi.
Unaweza kuwekeza penzi lako kwa mtu ambaye anajifanya kafa, kaoza kwako kumbe hana lolote.
Anajifanyisha tu na ukifanikiwa kuufungua moyo wako unaweza kushangaa wewe huna nafasi kabisa. Ndiyo maana nikasema ukipenda na ukapendwa kwa dhati ni bahati sana.
Wakati ikiwa hivyo, kuna tabia f’lani ambayo baadhi ya watu wanayo ya kutotaka kuwaona wenzao wakipendana. Yaani wapo ambao wanapenda kuona ndoa za wenzao zinatawaliwa na migogoro, wapo wanaowaendea wenzao kwa waganga ili waachane lakini pia kuna wanaofanya kila aina ya fitina ili mradi tu wawaone f’lani na f’lani hawako pamoja.
Huenda hata wewe imeshawahi kukutokea kwamba mtu wako wa karibu anamueleza mpenzi wako maneno ya umbeya ambayo ukiyachunguza unagundua yana lengo la kuwagombanisha tu.
Hebu jiulize, yule ambaye mara nyingi huenda kumwambia mpenzi wako kwamba amekuona sehemu na mtu ana nia gani hasa kama siyo tu kutaka kuchafua hali ya hewa?Halafu jiulize akishafanya hivyo yeye atanufaika nini? Ukifuatilia utagundua hana anachopata zaidi ya ile roho mbaya tu ya kutaka kuwaharibia wenzake.
Yaani yeye hajampata wa kumpenda basi akiona wenzake wanapendana inamuuma na anaona njia sahihi ya kujifariji ni kufitinisha tu. Hakuna jambo baya kama hili na kama wewe unayesoma una tabia hii, ujue unakosea sana na inaweza kuwa laana kwako ya kukufanya kila mtu akuone hufai kuwa mpenzi wake.
Kuna kisa ambacho kimemtokea dada mmoja ambaye ni jirani yangu kinachoendana na mada hii. Yeye ana mume wake na wamekuwa wakipendana sana.Upendo wao umewafanya hata Mungu awaangazie, kila kukicha wamekuwa wakipiga hatua za kimafanikio. Kumbe mmoja wa majirani wa wanandoa hao hafurahii ile hali. Baada ya kutafakari akaona njia sahihi ni kuwatibulia. Akanunua line mbili za simu, line ya kwanza akawa anaitumia kutuma sms kwa mwanamke akionesha yeye ni mpenzi wake na nyingine akawa anatuma sms kwa mume akijifanya ni msamaria mwema.
Siku ya kwanza akawa amemtumia mume wa yule dada kuwa, yeye ni jirani mwema na anaumia sana kumuona mumewe anatembea na kijana mmoja mtaani. Mume alipopata ile sms akaumia sana lakini akaamua kuchunguza kwanza.
Wakati anachunguza, yule mfitini akawa anatumia ile line nyingine kumtumia sms za kimapenzi yule mke wa mtu, meseji ambazo mtu yoyote akiziona anaamini ni wapenzi. Mbaya zaidi wakati mume anafuatilia zile taarifa za mkewe kumsaliti, siku moja akabamba sms kwenye simu ya mkewe inayotoka kwa yule jirani anayejifanya ni mwanaume akimtaka wakutane gesti kama kawaida yao.
Mwanaume huku akiwa tayari ana umbeya kwamba mkewe anamsaliti, akajua meseji hiyo haijapotea njia. Mzozo ukaanza, mume akatishia kutoa talaka lakini badaye uchunguzi ulipofanyika ikabainika aliyekuwa anafanya mchezo huo ni jirani yao kwa nia ya kuvunja ndoa.
Tukio hilo ni mfano wa michezo mingi ya kifitina unayochezwa na watu wenye roho za kwa nini. Yaani mtu na akili zake anatumia muda mwingi kujiuliza kwa nini mnapendana sana? Bila kufahamu kwamba sababu ya kupendana kwenu ni penzi la dhati mlilonalo, atawapaka matope kwamba mnaringa na maneno kama hayo, hii siyo poa kabisa.
Ninachotaka kukifikishwa kwako leo msomaji wangu ni kwamba, fitina ni mbaya. Kama wewe hujajaaliwa kuwa na mpenzi anayekupenda, endelea kumuomba Mungu ukiamini ipo siku atakujaalia.Maumivu yako ya kutopendwa isiwe sababu ya kuwaharibia wenzako ambao wameapia kufa na kuzikana. Kumbuka endapo utahusika kwenye kuwaachanisha watu waliotokea kupenda kwa fitina zako, Mungu hawezi kukuacha hivi hivi.

0 comments: