NI SIMANZI!! DENTI 'FORM FOUR' ALIYEFARIKI DUNIA SAA 3 KABLA YA MTIHANI

NI SIMANZI! Msichana Yunis Festo aliyekuwa na umri wa miaka 18 akisoma kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Simba wa Yuda iliyoko katika Kijiji cha Bulima, wilaya ya Busega mkoani Simiyu, alifariki dunia ghafla, saa takriban tatu tu kabla ya kuanza mitihani ya kumaliza elimu ya sekondari, alfajiri ya Jumatatu wiki hii.
Yunis Festo enzi za uhai wake.
Akizungumza kwa njia ya simu na gazeti hili akiwa Busega, mmoja wa walimu wa shule hiyo, Damian Kageba Lupimo alisema kabla ya umauti kumfika, wiki moja nyuma alikuwa amelazwa katika zahanati iliyopo kijijini hapo, hali iliyowalazimu wazazi wake kuja kumchukua na kumpeleka Mwanza kwa matibabu zaidi.
“Marehemu alikuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa Sickle Cell, lakini haikuwa siriaz sana, alirejea hapa shuleni Oktoba 31 mwaka huu.
Mwili wa Yunis Festo ukiagwa kwa ajili ya mazishi.
Alihudhuria mahafali pamoja na wenzake Novemba Mosi na siku iliyofuata baba yake aliondoka kurudi nyumbani,” alisema mwalimu huyo na kuongeza kuwa usiku wake, akiwa bwenini na wenzake, hali yake ilianza kubadilika.
Alisema baada ya kuona mabadiliko hayo, wanafunzi wenzake walijumuika naye usiku huo wa saa tisa katika kufanya maombi, lakini saa moja baadaye, walilazimika kumkimbiza katika zahanati ya kijiji baada ya hali yake kuzidi kuwa mbaya.
Baadhi ya wanafunzi wenzake wakiwa na simanzi.
“Saa 11 alfajiri Yunis aliaga dunia na alisafirishwa siku hiyo hiyo kwenda nyumbani kwao katika kijiji cha Lijembe kilichopo Kwimba mkoani Mwanza ambako alizikwa Jumatano hii,” alisema mwalimu huyo.
Yunis Festo alizaliwa Februari 26, 1996 na kifo chake kimeleta simanzi kubwa kwa wanafunzi wenzake wa shule hiyo inayomilikiwa na Mchungaji Jofephares Mtebe yenye kuanzia shule ya msingi hadi kidato cha sita.

0 comments: