UKAWA WAELEZA UTARATIBU WA KUPATA WAGOMBEA WAO.... WASAINI MUONGOZO WA USHIRIKIANO BILA NLD
Umoja
wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), umesaini muongozo wa ushirikiano katika
uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji; makubaliano ambayo
yatatumika kwenye uchaguzi huo uliopangwa kufanyika mwezi ujao.
Muongozo
huo ulisainiwa jana jijini Dar es Salaam na viongozi wa vyama
vinavyounda umoja huo ambao ni Profesa Ibrahim Lipumba (CUF), Dk.
Wilbrod Slaa (Chadema) na James Mbatia (NCCR-Mageuzi) wakati Emmanuel
Makaidi wa NLD alishindwa kusaini kwa kuwa alipata udhuru.
Profesa
Lipumba alisema miongoni mwa mambo ya msingi ni kusimamisha mgombea
anayekubalika zaidi katika kijiji, kitongoji au mitaa; kuangalia chama
kinachofanya vizuri katika eneo husika kwenye uchaguzi uliopita na idadi
ya wanachama.
“Kila
chama kilicho kwenye ushirika kinapaswa kuandaa wagombea (Mwenyekiti na
wajumbe) wenye sifa na wanaokubalika katika jamii isipokuwa ni marufuku
kwa chama kushawishi mwanachama wa chama kilichopo kwenye ushirika wa
Ukawa kuhamia chama kingine,” inaeleza sehemu ya makub aliano hayo.
“Vyama
vya ushirikiano vitatumia utaratibu wa mashauriano/muafaka katika
kumpata mgombea wa mtaa/kijiji/kitongoji kwa kuwashindanisha wagombea
kutokana na sifa na kukubalika kwao.”
Aidha,
makubaliano hayo yanaeleza pia kuwa sehemu ambayo serikali ya kijiji,
kitongoji au mtaa inayomaliza muda wake inaongozwa na mojawapo ya vyama
vilivyopo kwenye ushirikiano inaweza kuwa kigezo cha kuachiwa kuendelea
kutetea kiti hicho kama bado chama husika kinakubalika.
Makubaliano
hayo pia yanaeleza kuwa iwapo vyama vikishindwa kupata maridhiano ya
uteuzi, wanachama katika eneo husika watapigakura ya kumpitisha mgombea
mmoja miongoni mwa wale waliosimamishwa na chama. “Ngazi ya Wilaya ya
vyama shirika itakuwa msimamizi wa zoezi hilo,” yanaeleza makubaliano
hayo.
Makubaliano
mengine ni kuvitaka vyama hivyo kushirikiana kumnadi mgombea
atakayepitishwa na kwamba baada ya uchaguzi, viongozi wa kitaifa
wataandaa kanuni ya pamoja itakayosimamia nidhamu kwa viongozi wote wa
serikali watakaokuwa wamechaguliwa.
0 comments: